×
KATIKA SEHEMU HII:
Msaada
Jinsi ya kukuza kampeni yako
Kushiriki kampeni yako na ulimwengu
Mojawapo ya faida za kufanya kampeni yako mtandaoni ni kwamba unaweza kuishiriki na watu wengi sana katika muda mfupi. Ni jambo rahisi -- kadiri unavyowaambia watu kuhusu kampeni yako, ndivyo unapata watia saini wengi zaidi. Zifuatazo ni njia kuu za kueneza habari kuhusu kampeni yako. Marafiki zako wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujibu kitu wanachoona tena na tena, kwa hivyo jihisi uko huru kutumia mbinu kadha wa kadha ya kati ya zifuatazo na kwa pamoja, badala ya kuganda kwa unayoipenda zaidi.
BARUAPEPE NI MBINU BORA BIN BARABARA
Baruapepe ndiyo njia muhimu zaidi ya kuwashirikisha watu katika kampeni yako. Imekuwa uti wa mgongo wa mafanikio ya Avaaz -- kwa miaka mingi, watu wengi zaidi wametia saini kampeni za Avaaz baada ya kutumiwa baruapepe na mtu wanayemfahamu kuliko kupitia njia yoyote nyingine. Kupitia baruapepe, unaweza kufikia watu na kuwapa habari kamili, sio tu maneno 140. Ikiwa una kampeni inayopeperushwa kwa sasa, bofya hapa ili kutumia mwongozo wetu wa kuandika baruapepe fanifu na kuishiriki na kila unayemjua.
MITANDAO YA KIJAMII HUTANDAZA HABARI
Kuchapisha kwenye Facebook na Twitter inaweza kuwa njia ya rahisi zaidi kushiriki kampeni yako na watu wengi unaowajua. Kwenye Twitter-- hakikisha kuwa umejumuisha lakabu zozote za mtumiaji ambazo zitawezesha jumbe zako kuonekana na mlengwa wako na lebo (hashtegi) zozote zinazovuma au mada ambazo zitasaidia watu wanaolijali suala lako kuuona mtwito wako. Na haidhuru kumwomba rafiki yako mwenye wafuasi mara 10 zaidi yako aupige jeki ujumbe wako ;)
JIUNGE NA MAZUNGUMZO NA MIJADALA MTANDAONI
Kuna njia nyingi za kuchapisha habari mtandaoni. Jaribu kuchapisha kwenye blogu yako au kuandaa chapisho la mgeni kwenye blogu ya mtu mwengine -- unaweza kueleza kwa kina zaidi, hata zaidi ya baruapepe, kwa vile mtu yeyote anayesoma amelitafuta chapisho mwenyewe na kwa hivyo ana shauku ya kujua mengi zaidi. Kwa hivyo usisite kuibinafsisha, kuongeza viungo, majedwali, maua, madaha na madoido. Unaweza kuwa mwanachama wa shirika fulani lililo na tovuti na huenda wakachapisha kampeni yako. Na ukiona habari inayohusiana na suala lako, zingatia kuchapisha kiungo cha kampeni yako katika sehemu ya maoni ya habari hiyo -- wasomaji wanaweza kutembelea ukurasa wa kampeni yako na mwandishi wa habari vilevile atajifunza kuhusu juhudi zako.
KUPITISHA WAKATI KWA BUSARA
Sote tumelifanya jambo hili -- kutazama orodha zetu za gumzo juu chini ili kuona watu wanasema nini. Iwe ni Skype, Gchat, AIM, au nyingineyo, kuweka kiungo na dokezo la kibinafsi katika ujumbe wako wa hali halisi ni njia nzuri ya kuwapa watu wanaobarizi mtandaoni jambo la maana la kufanya.
KUPATA WAFUASI KWENYE JUKWAA NA ORODHA MBALIMBALI
Mojawapo ya changamoto katika kukuza kampeni yako ni kuwapata watu wenye shauku ya kushughulikia suala lako. Kuzingatia jinsi watu walivyojikusanya katika vikundi mbalimbali kulingana na mambo wanayoyajali au mada mahususi wanayopenda kujadili kutakurahisishia kazi. Tafakari kuhusu vikundi vinavyokujumuisha wewe (shirika, timu ya michezo, chama cha wataalamu, n.k.) au jaribu kutafuta orodha za watu mitandaoni wanaoangazia suala lako. Tovuti za mijadala mtandaoni, jukwaa ambazo watu hujadili mada fulani, pia ni mahali pazuri pa kupekuapekua. Huenda ikawa usijue kila mmoja katika orodha utakazozipata, lakini hilo ni jambo zuri -- kuwasiliana na watu ambao hujawahi kukutana nao lakini wanaolijali suala lako ni muhimu katika kukuza kampeni yako.
... na bila shaka ...
MAKINIKIA KAMPENI YAKO!
Tunasema chema chajiuza, sio? Huenda ikaonekana kama jambo lisilohitaji hata kutajwa, lakini mbinu bora zaidi ya kupata saini ni kuanza na kampeni murua au kali kabisa! Na ingawa usambazaji wa kampeni unaoufanya ni muhimu katika kupiga hatua mbele, kampeni yako hukua hususan wakati watu ambao hujawahi patana nao wanapoanza kuishiriki katika mitandao YAO. Mambo madogomadogo kama vile kukichonga na kukinoa kichwa cha kampeni yako vilivyo, kubuni ujumbe mjanja na mcheshi wa twitter unaowalenga watia saini, au kuchagua picha mufti bin murua kunaweza kusaidia kampeni yako ishirikike zaidi. Usihangaike sana katika kuifanya kampeni yako iridhishe kikamilifu kabla ya kutiwa saini na mtu yeyote, lakini kaa macho na kuwa tayari kuiboresha unapoona njia ya kufanya hivyo.
Anzisha kampeni yako
Jukwaa jipya la Kampeni za Jumuiya ya Avaaz linasaidia maelfu ya watu kuanzisha na kushinda kampeni, katika ngazi za kikata, kitaifa na kimataifa!